Wednesday, August 31, 2011

Rais wa Zanzibar Dk.Ali Shein Ahudhuria Swala ya Idd el Fitri Bwawani Hotel Zanzibar


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk Ali Mohamed Shein,akiwahutubia wananchi na waislamu katika baraza la Iddi el Fitri lililofanyika huko ukumbi wa Salama hall Bwawani Hotel mjini Zanzibar.
Makamo wa kwanza wa Rais Seif Sharif Hamadi akisalimiana na Waziri wa katiba na Sheria wa Zanzibar Abubakari Khamis Bakari baada ya kuingia katika kiwanja cha maisara mjini zanzibar kwa ajili ya kuswali swala ya Idi Elfitri.
Rais wa Zanzibar Alhaji Dr,Ali Mohd Shein pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali na wananchi,wakiwa katika swala ya iddi ambayo imeswaliwa kitaifa katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar.
Baadhi ya kinamama waliohudhuria katika swala ya Idi Elfitri huko katika kiwanja cha Maisara mjini Zanzibar
 Wananchi mbalimbali wa Zanzibar wakisikiliza hotuba ya Idi Elfitri baada ya kumaliza kuswali swala ya Idi huko katika kiwanja cha maisara zanzibar.Picha na Ramadhan Othman wa Ikulu -Zanzibar

Monday, August 29, 2011

Mbunge Wa Mvomero Aingilia Kati Mgogoro Wa Ardhi Kipera

|
Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Amos Makala akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero, Morogoro mwishoni mwa wiki katika harakati za kutatua mgogoro wa ardhi uliopo kijijini hapo , kufuatia mwekezaji Raia wa kigeni kuuziwa eneo kubwa la ardhi na kumega sehemu ya mashamba yao, kufunga barabara, shule na kubomoa baadhi ya vyoo vya wakazi wa kijiji hicho. MBUNGE wa jimbo la Mvomero, mkoani Morogoro, Amos Makala ameingilia kati mgogoro wa ardhi uliopo katika Kitongoji cha Kinyenze , Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali , Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro baina ya wananchi na mwekezaji wa Kigeni aliyeuziwa shamba kijijini hapo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki Kijijini hapo Makala aliyeambatana na Ofisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Majaliwa Jaffari amewataka idara ya ardhi kuchukua hatua za haraka na dharula kutatua mgogoro huo kabla ya kuibuka kwa machafuko ya uvunjifu wa amani.

“Nimejionea mwenyewe baada ya kusikia kiliochenu juu ya mwekezaji huyu, watu wa ardhi tafadhalini sana lishughulikieni suala hili haraka sana na mkae pamoja mgogoro huu umalizike upesi iwezekanavyo, ndani ya wiki moja tatizo hili liwe limemalizika”, alisema Makala.

Aidha Makala amesema tatizo hilo likiendelea ataungana na wananchi wake kufungua kesi Mahakamani ya kumpinga mwelezaji huyo na amemwomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero kutumia mamlaka waliyonayo kufika kijijini hapo wafungue uzio huo uliowekwa na mweklezaji huyo haraka ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali, watoto kwenda shule na watu kuvuna mazao yao yanayoibiwa na walinzi wa kampuni ya Tanbreed Poultry Limited ambayo imemega mashamba yao.

“Katika hili ninaungana nanyi na Viongozi wa Mkoa na Wilaya wafike hapa wakiwa na dola na kukata uzio huu, ili wananchi muendelee na shughuli zenu za kijamii, si haki kufunga barabara mnayoitumia kwenda katika makazi yenu na mashambani, hili lisipofanyika tutatafuta mwanansheria na kufungua kesi ya Mahakamani ya kumpinga mwekezaji huyu”,alisema Mbunge Makala.

Makala pia aliwapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kuwa watulivu pasipo kufanya vurugu katika kipindi kirefu tangu kuibuka kwa mgogoro huo bila kupatiwa ufumbuzi kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu licha ya kuandikiwa barua tangu mwezi Aprili mwaka huu mgogoro huo ulipoanza kushika kasi.

“Wananchi mmefanya jambo jema sana la kuheshimu mamlaka za kisheria kwa kuwa watulivu kipindi chote lakini vinginevyo hapa machafuko yangetokea maana wananchi mpo wengi kuliko hao askari wao wanaolinda hilo shamba”, alisema Makala.

Pia alisema kwa maelezo aliyoyasikia kutoka kwa baadhi ya wazee wa kijiji hicho Ally Kidunda na Said Ahmad na viongozi wa Kijiji yaliyotolewa kwaa nyakati tofauti Mwekezaji huyo ndiye mvamizi wa eneo lao na si wananchi maana hata kijiji hakimtambui kwa maana hajawahi kufika kwao.

Nae Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Mvomero, Majaliwa Jaffari alisema watalishughulikia suala hilo haraka na hasa baada ya kufika eneo la tukio na kukiri kuna mapungufu katika ramani waliyonayo.

Agosti 23, mwaka huu wananchi hao waliitaka serikali kuingilia kati mgogoro huo haraka kabla ya machafuko kutokea wakati wakiwa katika mkutano wa hadhara uliokuwa uhudhuriwe na Mkurugenzi wa Wilaya na Maofisa wa Ardhi. Habari na Picha:Mroki Mroki

Monday, August 15, 2011

SOBER HOUSE YATEMBELEWA NA MAAFISA WA MADAWA YA KULEVYA



Mmoja katika vijana waliopo Sober akielezea uamuzi wake wa kujiunga na Sober House kuachana na madawa na jinsi anavyoendelea kupata ushauri nasaha, dawa pamoja na maelezo
Viongozi waadamizi wa kitengo cha Madawa ya kulevya wakisikiliza kwa utulivu maelezo yaliyotolewa na waratibu pamoja na waathirika wa madawa ya kulevya katika ziara yao kujifunza jinsi ya kupunguza matumizi ya madawa Zanzibar
Vijana wa Sober house tawi la Tomondo wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa waandamizi wa madawa ya kulevya.
Mimi pia nikuwepo wakati wa picha ya pamoja pamoja na kamkoba changu kwani nilipomaliza tu nilikimbilia kwenda kutafuta futari.Picha Zote na Mdau Othman Mapara

Friday, August 12, 2011

Adha Ya Mgomo Wa Wauza Mafuta

Treni yasitisha safari kwenda bara
*Nauli, vyakula mikoani bei zapanda
*Wachumi watabiri hali mbaya zaidi
UPUNGUFU wa mafuta katika maeneo mbalimbali nchi umezidi kukolea na kusababisha athari mbalimbali za kiuchumi, ikiwamo kusitishwa kwa safari za treni ya kati, kupanda kwa nauli na bei za vyakula, huku wachumi wakitabiri hali mbaya zaidi.
Safari za treni kusitishwa
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imesitisha safari za treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda bara kutokana na kukosa mafuta.
Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo, Bw. Midladjy Maez alisemsa jana kuwa kutokana na hatua hiyo, treni iliyokuwa imepangwa leo saa 10:00 jioni kwenda bara na iliyopangwa kuondoka Tabora kwenda Mpanda kesho hazitakuwapo.


"Kampuni imeamua kusitisha safari za treni za abiria kwenda bara kutokana na maghala yetu kukosa mafuta ya kutosha, hivyo safari zitarejea endapo zitapata mgawo wa kutosha wa nishati hiyo," alisema Bw. Maez.
Aliwataka watu wote waliokata tiketi za kuondoka kwenda maeneo hayo kuonana na wakuu wa vituo ili kurejeshewa nauli zao, huku akiomba wawe wavumilivu katika kipindi hiki kutokana na usumbufu wanaoupata.
Mbeya nauli juu
Tatizo hilo la mafuta nchini limechukua sura mpya baada ya wamiliki wa daladala mkoani Mbeya kupandisha nauli kutoka sh. 350 mpaka 500 kutokana na nishati hiyo kupandishwa hadi sh. 3,000 kwa lita moja.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, wakazi wa eneo la Uyole jijini Mbeya walisema kuwa kiwango hicho cha nauli kimepanda bila kuzingatia utaratibu huku magari mengine yakishindwa kufanya kazi.
Mkazi wa Uyole, Bw. Ablahamu Kazubele alisema kuwa nauli ya awali kutoka Uyole kwenda mjini ilikuwa sh. 350 na sasa imekuwa sh. 500 ambayo si ya kawaida.
Dereva wa daladala inayofanya kazi zake kati ya Uyole na Igawilo maarufu kwa jina la Mwagito alisema kuwa wao wamelazimika kupandisha nauli kutokana na mafuta kupanda bei hadi sh. 3,000 kwa wachuuzi mitaani.
Vyakula vyapanda bei Songea
Mkoani Ruvuma, mgomo huo umesababisha kupanda bei kwa kilo ya unga kutoka sh. 600 hadi 1,500 na mchele kutoka sh. 1,000 hadi sh. 1,500 katika manispaa ya Songea.
Bw. Rashidi Hussein mkazi wa eneo la Mpambalioto mjini hapa alisema kuwa tatizo la kutokuwepo kwa dizeli na petroli limeleta athari kubwa, hasa kwa waumini wa dini ya kiislamu ambao kwa sasa wako katika mfungo wa Ramadhani.
Naye Bw. Didas Lyakulwa maarufu kwa jina moja la Mabrandi, alisema:
“Ndugu waandishi leo nimenunua mafuta ya petroli lita mojash. 5,000 badala ya sh. 2,135 kwa lita, kwa ajili ya kuweka kwenye jenereta ninalotumia kwenye biashara yangu ya baa na hoteli, hivyo kupata hasara kubwa,” alisema Bw. Lyakulwa.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Christine Ishengoma alisema tayari ameshawaagiza wamiliki wa vituo vyote vya mafuta mkoani humo wahakikishe kuwa mafuta yanapofika wayauze kwa bei halali, vinginevyo watachukuliwa hatua.

Wachumi watabiri mabaya
Wakati huo huo, wachambuzi wa masuala ya uchumi na siasa wametahadharisha kuwa kama tatizo hilo na mgawo wa umeme havitatatuliwa kwa njia sahihi, uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja utaendelea kuporomoka.
Wachumi hao wamesema kuwa wananchi wajiandae kwa hali ngumu ya maisha, ikiambatana na ukosefu wa ajira kuliko ilivyo sasa.Profesa Samuel Wangwe alisema kuwa ni wakati mwafaka sasa serikali ijue kwa undani namna biashara ya mafuta inavyoendeshwa, ili siku nyingine isikurupushwe kama inavyoonekana kutokea hivi sasa.
"Kama hali hii itaendelea, kwa kweli kutakuwa na tatizo kubwa, vitu kutofika, gharama za kusafirisha, kupanda kwa bei za vitu...hili la ulanguzi linaloonekana sasa ni matokeo tu ya upungufu huu wa mafuta.
"Lakini ni vyema serikali ikaijua vyema biashara hii, si kama sasa hivi ambapo inaonekana imekuwa taken by surprise. Waelewe biashara hii inakwendaje, imekaaje, wajue serikali inapaswa ku-play role gani hasa katika biashara ya mafuta, wadhibiti wakiwa na taarifa kamili ya nini kinafanyika. Wajifunze katika hali kama hii, nchi zingine kama Ujerumani, Sweden, Marekani au Uingereza zinafanyaje katika kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi.
Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba alisisitiza kauli yake amabyo amekuwa akiitoa mara kwa mara juu ya ombwe la uongozi, ambalo alisema limekuwa likionekana katika serikali iliyoko madarakani, akiongeza kuwa kama ufumbuzi sahihi hautapatikana kwa wakati mwafaka taifa na wananchi kwa ujumla watakuwa katika matatizo makubwa kuliko ilivyo sasa.
Prof. Lipumba ambaye yuko katika mapumziko ya kujenga afya yake baada ya kufanyiwa operesheni nchini India hivi karibuni, aliungana na Prof. Wangwe, akisema kuwa kama hakutakuwa na suluhisho la haraka, kutakuwa na mfumuko mkubwa bei kuliko ilivyo sasa, hivyo kusababisha hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu.
"Tatizo ni hilo hilo ambalo mara kwa mara tumelisema, bahati mbaya na ninyi ujumbe mmekuwa hamuufikishi sawa sawa kama inavyotakiwa. Suala la mafuta limedhihirisha ombwe la uongozi ambalo nimekuwa nikisema. Suala la kupunguza bei lilifanywa kisiasa zaidi kwa ajili ya kujipatia umaarufu. Inavyoonekana serikali haikufanya utafiti kabla, kuwasiliana na wauzaji kabla ya bajeti.
"Serikali ilipaswa kujua mapema kuwa utaratibu mpya hautakuwa na athari yoyote...leo kuna mtu kaniambia bei za bajaj zimepanda, sasa mafuta yanaanza kuuzwa kwa bei ya magendo kwa bei ya kuruka...matatizo yatakuwa makubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Hakuna sheria inayowapatia EWURA mamlaka ya kupanga bei, wanaweza kutoa bei elekezi tu, ingawa pia wauzaji hawaruhusiwi kupanga njama za kuuza bei kubwa maana hiyo ni jinai.
"Kwa sababu hakuna price control huwezi kuwashtaki, bali unaweza kuwanyang'anya leseni wasiuze mafuta tena. Lakini serikali ilipaswa kulifanyia suala hili utafiti kabla hata ya bajeti, kujua kama uamuzi huo ungeweza kuongeza matatizo zaidi. Serikali lazima ifanye mambo kwa uhakika. Na katika hali ya sasa ujue hata meli zinaweza kuelekezwa kupeleka mafuta sehemu nyingine badala ya kuleta Tanzania, hivyo tukaendelea kuwa katika matatizo makubwa."
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. John Heche alidai kuwa anazo nyaraka zinazoonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina mikataba ya kibiashara na baadhi ya makampuni ya mafuta, ndiyo maana hakiwezi kukemea hali inayoendelea nchini, huku pia akisema kuwa baadhi ya wabunge na mawaziri wana mgongano wa maslahi katika tatizo hilo.
"Ninazo nyaraka, nitazitoa wakati mwafaka, CCM wana mikataba ya kibiashara na baadhi ya makampuni ya mafuta, mmoja una kiasia cha sh. bilioni 3. Hiyo ni mbali na kuwa uongozi wa sasa wa serikali ya CCM uliingia kwa ufadhili wa fedha za makampuni hayo, ndiyo maana mpaka sasa hatujasikia kauli 'serious' juu ya suala hili.
Akizungumzia shutuma hizo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Bw. Nape Nnauye alisema "mwambieni Heche azitoe hizo nyaraka, maana sasa hivi ndiyo wakati mwafaka, suala la mafuta linazungumzwa sana, atoe tu. Sisi tunaweza kutoa mikataba yote, ingawa unaweza kumtafuta Mwigulu Nchemba, maana yeye ndiyo hasa anahusika na Idara ya Fedha na Uchumi, anaweza kukwambia mengi.
"Lakini hayo ni maneno ya kihuni, yamekuwa yakitolewa na watu mbalimbali, nimeyaona hata mtandaoni...lakini hata maneno kuwa hatujachukua hatua...ukiuliza sisi ndiyo tulikuwa tunahangaika kuhakikisha mambo yaende. Mpigie Mwichemba atazungumza zaidi."
Majira lilimtafuta Bw. Nchemba kwa simu yake ya mkononi lakini ilikuwa ikiita bila kupokewa, hivyo ikalazimu kumtumia ujumbe mfupi, kumwomba azungumzie shutuma hizo, lakini hatukupata majibu hadi tunakwenda mitamboni.
Imeandikwa na Esther Macha, Mbeya; Cresensia Kapinga, Songea; Tumaini Makene na Grace Ndossa.

Thursday, August 11, 2011

Matukio Bungeni ...


Zainab Kawawa (shoto) vitimaalum (kulia) Angelah Kairuki (CCM) vitimaalum wakiteta...

Waziri Mkuu (mwenyetai ya zambarao) akiongea na wasanii Bungeni ...

Mdau wa Habari Neville Meena (kulia) akimpongeza waziri nchmbi katika viwanja vya bunge. Picha zote; Mwanakombo Jumaa, HABARI MAELEZO

Tuesday, August 9, 2011

Rais Wa Somalia Atua Tena Tanzania

Rais Jakaya Kikwete (kulia) akikumbatiana na mgeni wake Rais Sheikh Sharif Ahmed wa Jamhuri ya Somalia alipowasili jana mchana kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini.
Rais Jakaya Kikwete na mgeni wake Rais Sheikh Sharif Ahmed wa Jamhuri ya Somalia wakipita katikati ya gwaride la mapokezi ya mgeni huyo mara baada ya kuwasiri kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Dr Shein Azindua Uchumaji Wa Karafuu ...

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohammed Shein akipima karafuu katika uzinduzi wa Uchumaji wa zao hilo huko Mkanyageni Pemba...


Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein akianika Karafuu pamoja na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui katika siku ya uzinduzi wa Uchumaji wa zao hilo Msimu huu huko Pemba.

Saturday, August 6, 2011

CCM Itarejesha Imani Ya Vijana, Na Kuwaeleza Ukweli Ulivyo-Nape


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kitahakikisha katika mabadiliko yake ya sasa kinawarejesha katika kuujua ukweli vijana waliopotoshwa na wapinzani hadi kufikia hatua ya kudhani hakuna mazuri yaliyofanywa tangu uhuru.


Mikakati hiyo ilisemwa jleo na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye wakati akizungumza na baadhi ya viongozi na watangazaji wa Clouds Media Group, Mikocheni Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kujitambulisha katika wadhifa wake huo na kueleza mabadiliko yaliyofanywa na Chama, mapema Aprili mwaka huu.


Alisema, wakati wapo vijana ambao hawakuipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu uliopita kwa sababu zinazoonekana kuwa za msingi, lakini ipo idadi kubwa ya vijana ambao walifanya hivyo kutokana na chuki tu kutokana na kushibishwa na uongo na baadhi ya vyama vya upinzani.


Nape alisema katika miaka ya karibuni hasa baada ya kupevuka kwa kiwango kikubwa mawasiliano kwa njia ya mitandao kwenye kompyuta, baadhi ya vyama hivyo vimetumia na vinaendelea kutumia mawasiliano hayo kueneza uongo kwa njia hiyo na kufanikiwa kuwanasa vijana wengi kwa kuwa ndio wanaopendelea zaidi kutumia mawasiliano hayo ya mtandao.


"Baada ya vyama vya upinzani kujua kwamba vijana wengi wanapenda zaidi upashanaji habari kwa njia ya mitandao kwenye kompyuta, kuliko mikutano ya hadhara na njia nyingine za kawaida,


baadhi ya vyama hivi vimetumia sana njia hii kuwajaza uongo vijana", alisema Nape.


"Na kwa sababu uongo ukizidi kuenezwa bila kupingwa huweza kuonekana ndiyo ukweli, baadhi ya vijana wameamini uongo huo, na matokeo yake wamejenga chuki kiasi cha kutoyaamini hata mambo ya maana na ya msingi wanayoambiwa na CCM na serikali yake jambo ambalo ni hatari kwa hatma ya taifa", alisema Nape.


Alisema katika mikakati yake ya sasa CCM itahakikisha inawapa ukweli kupitia njia hiyo ya mawasiliano ya mitandao ya kwenye kompyuta kama 'face book' na kueleza matumaini yake kwamba hatua hiyo itazaa mafanikio kwa kuwa yameanza kuonekana katika hatua za awali ambazo CCM imeanza kufanya.


Nape alisema, CCM inafanya hivyo kwa kuwa bado kina uwezo wa kuongoza huku kukiwa hakuna chama cha upinzani ambacho kinaweza kujitapa kuwa kinaweza kuongoza nchi kwa uhakika ikilinganishwa na hali inayojionyesha katika vyama hivyo hadi sasa.


Alisema, mbali ya kuyaendea makundi ya vijana, CCM pia imejipanga kuyafikia kwa ufanisi zaidi makundi yote, kwa kutumia njia mbadala, ikiwemo kufuatilia kwa karibu maoni ya vyombo vya


habari hasa vile vinavyoonekana kuwa makini zaidi katika kutoa habari zake.


Nape aliahidi CCM kutoa ushirikiano mkubwa kwa vyombo vya habari katika kuhakikisha vinapata habari za ukweli, sahihi na kwa wakati kuhusu chama na hata za ndani ya serikali.


"Tunaamini sisi CCM tukifungua masikio yetu vilivyo kwa vyombo vya habari tuyaweza kuongoza nchi kwa usahihi zaidi, kwa sababu ninyi vyombo vya habari ndiyo mliopo mitaani wakati mwingi, hivyo mnaweza kuwa mnayajua mengi kuliko sisi, ni vizuri tukawa tunawasikiliza na kufanyia kazi mnayosema", alisema Nape.


Katika ziara hiyo, Nape alizungumzia kwa kina dhana ya mabadiliko ndani ya Chama na utekelezwaji wake unavyoendelea na baadaye waandishi wa Clouds Media Group walipata fursa ya


kuzungumza na kumuuliza maswali yaliyoona yanafaa.


Baadaye Nape akiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni hiyo ambayo ni walimiki wa vituo vya Clouds FM, Choice FM na Clouds TV, Ruge Mutahaba alipata fursa ya kutembelea baadhi ya vituo hivyo kuona kazi zinavyofanyika.

Balozi Wa Zambia Nchini Amtembelea Rais Wa Zanzibar Dk Ali Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akifuatana na mgeni wake Balozi wa Zambia nchini Tanzania Mama Mavis Lengalenga Muyunda, aliyefika Ikulu Mjini Zanzibar Leo kuzungumza na Rais
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akisalimiana na Balozi wa Zambia nchini Tanzania Mama Mavis Lengalenga Muyunda aliyefika Ikulu Mjini Zanzibar Leo.Picha na Ramadhani Othman,Ikulu-Zanzibar

Thursday, August 4, 2011

Mhe.Lowasa Ziarani India



Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa


MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa (katikati kulia) akiwa katika kikao cha pamoja na Wabunge wa Bunge la India wanaoongozwa na Spika wa Bunge lao, Lok Sabha . Kikao hicho kilifanyika New Delhi India ambako kamati hiyo iko katika ziara ya kikazi.

Tuesday, August 2, 2011

Bada Ya Kamati Kuu Ya CCM Kulalamikia Bei Ya Mafuta, Bei Za Mafuta Zapungua

Serikali imepuguza bei ya mafuta ili kuwapunguzia makali watumiji wa badhaa hiyo nchini.


Akizungumza na wanahabari Mkurugenzi wa EWURA Haruna Masebu amesema mafuta ya petrol yamepungua kwa sh 202.37 sawa na asilimia 9.17 ambapo mafuta ya dizeli yatakuwa yamepugua kwa shilingi 173 ambay ni sawa na asilimia 8.32.


Bwana Masebu alisema alisema bei ya mafuta ya taa imeshuka kwa shilingi 181.37 sawa na asilimia 8.70 na mabadiliko hayo yametokana na marekebisho ya yaliyofanywa na kanuni kukokotolea bei za mafuta.


Alisema bei zingeshuka kwa sababu ya kupanda kwa bei katika soko la dunia na kuendelea kushuka kwa tahamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani.


Aidha Masebu alisema, kwa mujibu wa Sheria ya mafuta ya mwaka 2008 bei za mafuta ya petrol I zitaendelea kupangwa na soko na EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo ya bidhaa za mafuta.


Alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petrol kwa bei ya ushindani pasipo kuongeza bei iliyopangwa na taasisi ya EWURA.


Pia vituo vya mafuta vimetakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana ili kuonyesha bei ya mafuta.


Kwa mujibu wa Bwana Masebu bei hiyo ya mafuta imeanza kutumika rasmi leo.

Ndugai Atetea Mikopo Ya Mashangingi


Amesema badala yake wakae pamoja na kupendekeza njia ambazo zinaweza kutumika serikalini ili ununuzi wa mgari katika idara na taasisi zake mbalimbali upungue kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na matumizi makubwa ya fedha za umma. Bw. Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), alitoa wito huo juzi katika mahojiano na gazeti hili Mjini Dodoma juu ya mashangini hayo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi. “Hamna mbunge hata mmoja ambaye anatumia fedha za umma kununulia gari la kufanyia kazi, iwe ni kutoka upinzani au chama tawala, kinachofanyika wabunge wote wanapewa mikopo ambayo inasimamiwa na Ofisi za Bunge kwa kuwapa dhamana wakati wa kwenda kukopa fedha hizo ili waweze kununua magari ya kufanyia kazi,” alisema na kuongeza: “Ofisi ya Bunge inahusika na dhamana tu, kinachofuatia ni mbunge kujaza fomu husika na kufuata taratibu zote za kukopa fedha za gari. Kwa safari hii zinatakiwa zisizidi sh. milioni 60, kati yake sh. milioni 45 ndizo wanakopeshwa na kupitia mishahara yake na posho zitakuwa zinakatwa kidogo kidogo hadi miaka mitatu awe amemaliza kurejesha,” alifafanua Bw. Ndugai. Alisema utaratibu unaotumika hapa nchini kwa kuwakopesha wabunge fedha za kununulia magari ya kufanyia kazi ni mzuri tofauti na nchi jirani kama Kenya na Uganda ambazo zinawapa bure wabunge wote kila mmoja gari lenye thamani ya sh. milioni 200. “Tumekuwa tukiwabebesha wabunge mizigo mizito mara kwa mara likiibuka suala la posho, magari, mishahara wao tu ndiyo wanaonekana wanapendelewa, lakini siyo kweli ndiyo maana serikali kwa kutambua nafasi yao katika kulitetea taifa inawajengea uwezo wa kujitegemea katika magari, kwa kuwa utaratibu wa kumkopesha mbunge gari inaipunguzia serikali gharama ya kununua magari mengi, gharama za matengenezo, mafuta na dereva wa kuwaendesha kwenda katika shughuli zao,” alisema Bw. Ndugai. Kuhusu magari ya serikali Alisema kama serikali itaanzisha utaratibu wa kuwakopesha watendaji wake fedha za kununulia magari yao binafsi ili ipunguze gharama, ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Wilaya na Mikoa, hatua hiyo itaokoa fedha nyingi za umma. “Nimewahi kutembelea katika Wizara moja ya Mazingira nchini Afrika ya Kusini nikakuta ina magari mawili tu kwa ajili ya dharura, lakini hapa nyumbani suala hilo halipo, hivyo ninaona kama tunaweza kuiga wenzetu kwa kuwakopesha fedha ambazo zitakuwa zinarejeshwa kwa awamu na hivyo kupunguza gharama serikalini kama Rwanda ilivyowahi kufanya kwa kuuza asilimia kubwa ya magari ya serikali,” alifafanua Bw. Ndugai. Bw. Ndugai aliongeza kuwa umefika wakati kwa kila mwananchi kuliamini bunge lao kwa kuepuka maneno ya upotoshaji ambayo wakati mwingine yanaweza kuwafanya kugawanyika katika makundi mbalimbali, bali washirikiane na wabunge wao katika kuwawasilishia kero zao ili zipatiwe ufumbuzi bila kujali itikadi zao za chama.Chanzo Gazeti Majira
NAIBU Spika, Bw. Job Ndugai amewataka wananchi kuacha kuwashambulia wabunge juu ya magari wanayonunua kwa mikopo kwa kuwa kufanya hivyo wanakuwa hawawatendei haki.

Monday, August 1, 2011

Taarifa Ya Maazimio Ya Kamati Kuu Ya CCM

|
Uongozi wa juu wa chama cha Mapinduzi CCM ukiwa katika kikao cha kamati kuu kilichomalizika jana mjini Dodoma.


Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imemaliza kikao chake cha siku moja usiku wa tarehe 31/07/2011 mjini Dodoma chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
Pamoja na mambo mengine Kamati Kuu imeamua yafuatayo;
1. Imefanya uteuzi wa makatibu ishirini na saba (27) kujaza nafasi zilizokuwa wazi katika wilaya hizo. (majina na wilaya zao yameambatanishwa). Pamoja na uteuzi huo, Kamati Kuu imetengua uteuzi wa Makatibu wa Wilaya watatu (3) katika kuboresha ufanisi wa kazi katika wilaya hizo.(majina na wilaya zao yameambatanishwa).
2. Kamati Kuu imepokea na kuridhia taarifa ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwakilisha Mkoa wa Tabora, Ndugu Rostam Aziz. Aidha imempongeza kwa uamuzi huo uliozingatia maslahi mapana ya chama chake.
3. Kamati Kuu imepokea pia taarifa ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Ndugu Rostam Aziz na kuagiza chama kupanga ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea ubunge wa Jimbo la Igunga itakayozingatia ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi juu ya uteuzi wa mgombea.
Aidha Kamati Kuu imeagiza shughuli zote za kampeni kutafanywa na CCM Mkoa, Wilaya na ngazi zote za chama wilayani Igunga. CCM Taifa watashiriki kuongeza nguvu. Chama kinatoa wito kwa wana CCM, wapenzi na wakereketwa wa chama chetu kushiriki kwa pamoja kuhakikisha jimbo linabaki kwa CCM.
4. Kamati Kuu haijaridhishwa na kiwango cha bei ya mafuta ya taa nchini kwa kuwa ndio nishati inayotumiwa na wananchi wengi wenye kipato cha chini. Aidha Kamati Kuu haikuridhishwa na maelezo ya kupandishwa kwa bei ya mafuta hayo kwa kisingizo cha kuzuia uchakachuaji wa mafuta mengine.
Hivyo basi, Kamati Kuu imeiagiza Serikali kutafuta njia za kushusha bei ya mafuta ya taa na kuvitaka vyombo vya Serikali vinavyohusika na usimamiaji wa ubora wa mafuta, vihakikishe vinatimiza wajibu wake kuzuia kabisa mtindo wa uchakachuaji wa mafuta nchini na si kupandisha bei ya mafuta ya taa kama suluhisho.
5. Kamati Kuu inasikitishwa na tatizo la umeme nchini kwani athari zake kwa uchumi wa Taifa na mtu mmoja mmoja ni kubwa. Hivyo basi imeitaka Serikali kutumia muda iliyopewa wa kurekebisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuja na mpango wa dharura wa kunusuru hali hii na kisha kulimaliza kabisa tatizo la umeme nchini.
6. Aidha Kamati Kuu imejadili masuala mengine kama; migogoro ya ardhi, tatizo la bei ya pamba, tatizo la uuzaji wa mahindi, migogoro migodini, masuala yanayohusu kero za Muungano na kuagiza Serikali kuyashughulikia kwani yanatatulika.
7. Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kazi nzuri ya kutekeleza maamuzi ya NEC na kuitaka iongeze kasi katika utekelezaji huo, ili kuhakikisha mageuzi yaliyokusudiwa yanatekelezwa kwa wakati. Aidha imejadili na kupitisha miundo mipya ya Idara ya Itikadi na Uenezi na Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.


8. Kuhusu suala la maadili ndani ya Chama, Chama kinaendelea kusimamia maadili, na kuwataka wale waliotakiwa kujipima na kuwajibika watumie muda huo, kujipima na kuwajibika kwa masilahi mapana ya chama.


idha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inatarajiwa kukutana wakati wowote mwezi Septemba, ambapo pamoja na mambo mengine itatathimini utekelezaji wa maamuzi yake.
Imetolewa na:-
ape M. Nnauye (MNEC)
KATIBU WA NEC, ITIKADI NA UENEZI
DODOMA
1/8/2011